Inasemwa kwamba...
*Arushwa kwa helikopta hadi Morogoro
*Asomewa mashitaka ya uchocheziKATIBU wa Taasisi na Jumuiya za Kiislam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro akiwa chini ya ulinzi mkali baada ya kuwasili katika uwanja wa Gofu mjini Morogoro kwa helikopta ya polisi. Ponda alifikishwa mahakamani Morogoro,
baada ya mapema asubuhi jana kuachiwa huru katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa shtaka la kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, kabla ya kukamatwa tena na polisi.
Akisoma mashitaka matatu dhidi ya Sheikh Ponda mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro Richard Kabate, Mwanasheria wa Serikali, Bernard Kongola akiwa na wanasheria wenzake wa serikali, Gloria Rwakibalira na Akisa Mhando, alidai Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Ponda alitoa maneno ya uchochezi.