Tuesday, August 20, 2013

Sheikh Ponda Mtuhumiwa ghali zaidi

Inasemwa kwamba...
*Arushwa kwa helikopta hadi Morogoro
*Asomewa mashitaka ya uchochezi
KATIBU wa Taasisi na Jumuiya za Kiislam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro akiwa chini ya ulinzi mkali baada ya kuwasili katika uwanja wa Gofu mjini Morogoro kwa helikopta ya polisi. Ponda alifikishwa mahakamani Morogoro,
baada ya mapema asubuhi jana kuachiwa huru katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa shtaka la kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, kabla ya kukamatwa tena na polisi.

Akisoma mashitaka matatu dhidi ya Sheikh Ponda mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro Richard Kabate, Mwanasheria wa Serikali, Bernard Kongola akiwa na wanasheria wenzake wa serikali, Gloria Rwakibalira na Akisa Mhando, alidai Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Ponda alitoa maneno ya uchochezi.


Alidai Ponda alisema: “Ndugu waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na watajitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti,f ungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana”.

Kongola alidai kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam iliyotolewa na Hakimu V. Nongwa Mei 9 mwaka huu ambayo ilimtaka Ponda kuhubiri amani ndani ya mwaka mzima.

Alidai maneno hayo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 124 cha mwaka 2002.

Katika shitaka la pili, Kongola alidai Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Ponda aliwaambia Waislam kuwa serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.

Mwanasheria wa serikali alidai Ponda aliwaambia Waislamu hao kuwa serikali haikupeleka jeshi Loliondo wananchi walipokataa mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao.

Alidai Ponda alisema serikali haikuepeka wanajeshi Loliondo kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristu, maneno ambayo yaliumiza imani za watu wengine.

Kongola alidai matamshi hayo ni kinyume na kifungu cha sheria 129 cha mwaka 2002.

Katika shitaka la tatu Kongola alidai kuwa matamshi ya Ponda aliyoyatoa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, ni kinyume na kifungu cha sheria namba 390 na kanuni ya adhabu namba 35 ya mwaka 2002.

Ponda alikana mashitaka yote matatu.

Mwanasheria wa serikali aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kutaka kesi ianze kusikilizwa Septemba 2 mwaka huu.

Hata hivyo upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kesi ianze kusikilizwa Agosti 26 mwaka huu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Kabate kuzipa pande hizo muda wa kujadiliana.

Baada ya kujadiliana kwa daakika tano walirejea mahakamani na kupanga kesi ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.

Mawakili wa upande wa utetezi, Ignas Pungwe na Bartholomew Tarimo walisema waliomba kesi isikilizwe terehe hiyo kwa vile mteja wao bado ni mgonjwa na anahitaji kupatiwa matibabu.

Awali baada ya Sheikh Ponda kuwasili kwa helikopta ya polisi katika uwanja wa Gofu alipakiwa katika gari maalum lililoongozana na magari mengine matatu ya polisi.

Mahakamani nako ulinzi umeimarishwa kwa Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) usalama wa taifa na mbwa wa polisi.

Baada ya kufika eneo la Mahakama saa 5.00 asubuhi magari yalisimama kwa takribani dakika 30 kabla ya askari kushuka na kumfungulia mlango Ponda ambaye aliingizwa mahakamani huku umati wa wananchi wakiwa wamefurika nje ya mahakamani hiyo.

Baada ya kesi kumalizika ulinzi uliendelea kuimarishwa hadi alipopandishwa kwenye gari maalum kuelekea kwenye helipokta iliyokuwa imeegeshwa kwenye Uwanja wa Gofu saa 6.00 mchana, tayari kwa safari ya kurejeshwa Dar es Salaam.

Chanzo:>Mwananchi.

No comments:

Post a Comment