Tuesday, August 20, 2013

MAANDAMANO YA CHADEMA KUMNG'OA MEYA ILEMELA JIJINI MWANZA YAISHA KWA MABOMU



MAANDAMANO ya amani yaliyokuwa yameandaliwa na chama cha demokrasia na maendeleo(chadema) yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji la Mwanza baada ya kuibuka mapambano makali baina ya waandamanaji hao na jeshi la polisi mkoani Mwanza na kusababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa chama hicho.



Maandamano hayo ya amani ambayo yalianzia katika eneo la Buzuruga nje kidogo ya jiji la Mwanza yalikuw ayakiongozwa na wabunge Highness Kiwia wa Ilemela pamoja na Ezekiel Wenje kuelekea katika viwanja vya Furahisha yalilenga kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa ya Ilemela kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.



Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza kutanda katika eneo hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye namba za usajili DK 068EXV aina ya Toyota Land Cruiser

Maandamano yakipita barabara ya Balewa kuelekea barabara ya Makongoro hatimaye viwanja vya Furahisha Kirumba Mwanza.


Mtaa wa jiwe kuu kata ya Kitangiri na ujumbe wao.


Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kana kwamba yangelimalizika salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa 5.38 huku yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya Uganda 779 UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha nzito ikiwa ni pamoja na mabomu ya machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa katikati ya maandamano hayo.


Askari polisi akiwaelekeza waandamanaji njia ya kuingia viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.


Walioacha shughuli zao za kila siku waliungana na wale ambao walikuwa shughulini kutafuta kipato kama mama huyu mstari wa mbele kwenye maandamano.




Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya Furahisha kwa amani,waandamani hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyosomeka kuwa ‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi yako ya awali, na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara kw amara kesi dhidi ya Matata na jingine lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji barua za kurejeshwa kwa madiwani wetu.


Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa maandamano hayo ya amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo,hakukuwa na kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo kupokea maandamano hayo.



Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa Serikali,viongozi wa chadema pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa dakika kadhaa kwa ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya waandamanaji kuwa wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Highnes Kiwia kwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya kuwaletea wananchi walioandamana juu ya hatima ya madiwani hao.

Chanzo:>GSengo

No comments:

Post a Comment